Sunday, April 21, 2019
Swahili > Maoni > Zimbabwe! Zimbabwe! Zimbabwe!

Zimbabwe! Zimbabwe! Zimbabwe!

Mgogoro Zimbabwe

Kumekuwa na sintofahamu nchini Zimbabwe tangu juzi. Kikosi Kikuu cha Inkomo kiliripotiwa kuondoka katika ngome yake na kuingia mjini na kuziba njia kuu.

Mkuu wa Majeshi alikaririwa akitoa onyo akiambatana na Wakuu Waandamizi 90 wa Jeshi la Zimbabwe. Umoja wa Vijana wa ZANU PF ulipaza sauti kulitaka Jeshi la Nchi kutoingilia siasa. Hatimaye imeripotiwa kuwa Jeshi limekitwaa Kituo cha Taifa cha Utangazaji huku taarifa zikiarifu kuwa Ikulu imezingirwa.

Jeshi limearifu zaidi kuwa halimlengi Rais Robert Mugabe bali linawalenga ‘wahalifu’ wanaomzunguka Rais huyo na kuharibu au kuyumbisha uchumi na ustawi wa nchi. Jeshi limearifu zaidi kuwa hali ya Rais na familia yake iko salama.

Mgogoro Zimbabwe
Umoja wa Vijana wa ZANU PF ulipaza sauti kulitaka Jeshi la Nchi kutoingilia siasa.

Hatuhitaji kuingilia mzozo wa ndani wa Zimbabwe wala sio kazi yetu kunyoosha kidole kuonyesha nani mkosaji na nani yuko sahihi. Nilopokuwa Uingereza mwanzoni na katikati ya miaka ya 2000 nilikutana na Wa-Zimbabwe wengi (Mashona na Mandebele) walioikimbia nchi yao kutokana na sintofahamu ya kisiasa iliyokuwa katika nchi yao.

Niliporejea nchini niliwakuta wengine hata huku. Wa-Zimbabwe ni ndugu zetu na ni binadamu wanaohitaji amani na utulivu katika nchi yao.. Watakaothirika zaidi katika vurugu zinazoendelea kule ni watoto, wanawake, wazee na wagonjwa. Ninatoa wito kwa wanaombi wote na Watanzania wote na Afrika yote kuiombea Zimbabwe.

Tuombe pia kwa ajili ya Kanisa nchini Zimbabwe ili lisimame katika nafasi yake na kuwa nuru katika saa na wakati kama huu. Tuombe ili mzozo unaoendelea Zimbabwe miongoni wanaoendesha nchi ile umalizike haraka na kwa amani.

Tuombe hekima ya Mungu miongoni mwa nchi nyingine ambao ni washika dau katika uchumi na siasa za Zimbabwe. Nchi yetu ni mdau mkubwa wa Zimbabwe. Tuombe hekima ya Mungu kwa ajili ya wanadiplomasia wetu wakiongozwa na Rais wetu Dkt. John Magufuli pamoja na marais wetu wastaafu.

Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula – Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania.