Sunday, April 21, 2019
Swahili > Maoni > Zimbabwe Nyuma Ya Pazia: Kwanini General Chiwenga Anacheka Na Mfungwa Wake?

Zimbabwe Nyuma Ya Pazia: Kwanini General Chiwenga Anacheka Na Mfungwa Wake?

Mgogoro Zimbabwe

Picha hiyo imeishangaza dunia. Kwamba Rais aliyepinduliwa na kuwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani ‘ House Arrest’, anatembelewa na kiongozi wa mapinduzi. Wanakaa kuongea, kunywa chai pamoja na kucheka.

Lakini, waliojitahidi kuifuatilia Zimbabwe kabla na baada ya uhuru watakubaliana nami, kuwa hilo si la ajabu kabisa.

Army General Constatine Chiwenga na Robert Mugabe ni marafiki. Ni makomredi waliofahamiana tangu zama za Chimurenga- Mapambano ya msituni kupigania uhuru wa Zimbabwe.

Kwanini Mugabe hakosi usingizi mbele ya akina Chiwenga?

General Chiwenga na makomredi wenzake hawawezi kamwe kumdhuru Robert Mugabe na kisha kuandamwa na laana ya kihistoria.

Si wengi wenye kufahamu, na wengine wanahitaji kukumbushwa, kuwa ukweli ni kuwa Robert Mugabe zamani kidogo alishawaambia makomredi wenzake ndani ya ZANU PF na kwenye Jeshi la Zimbabwe akiwemo Army General Chiwenga, kuwa angependa kuondoka.

Nyuma ya pazia, iko kwenye rekodi, kuwa ni jeshi la Zimbabwe ndilo limemng’ang’aniza Mugabe asiondoke madarakani. Ilikuwa ni mwisho wa mwezi Machi mwaka 2008. Ni baada ya kujulikana matokeo ya uchaguzi kuwa Morgan Tsvangirai kura zake zilitosha kuingia Ikulu.

Kwenye mkutano wake wa siri na majenerali inasemwa Robert Mugabe aliwaambia makomredi wenzake kuwa yuko tayari kuachia ngazi. Ndipo pale Mkuu wa Majeshi, General Chiwenga akamwamuru Mugabe asiyakubali matokeo. Akaambiwa atulie Ikulu na mengine awaachie jeshi.

Jambo hili linaandikwa na mwandishi mahiri kutoka Sweden, Bw. Stig Holmqvist kwenye kitabu chake. (Pa Vag Till Presidenten, ukurasa wa 300). Kimeandikwa kwa lugha ya Kiswidi ikiwa na maana ya ‘ Njiani Kwenda Kwa Rais’. Nina bahati ya kukutana na mwandishi huyo ambaye pia amepata kukutana na Robert Mugabe.

Hakuna shaka kuwa Jeshi ndilo limekuwa likimcontrol Mugabe kwa muda mrefu sasa. Yawezekana kabisa, hesabu za makomredi akina Chiwenga na wenzake, watu wa aina ya Emerson Munangagwa zimevurugwa na alichokionyesha Grace kuwa amedhamiria kweli kuchukua madaraka na hata kuwa na nguvu za kumshawishi Robert Mugabe kumwondoa kwenye Umakamu wa Rais Munangagwa.

Katika mazingira hayo, haishangazi kuwa Robert Mugabe hana wasiwasi wowote na anaweza kusinzia, kulala na hata kukoroma mbele ya waliomwambia kuwa abaki tu madarakani wakati alitaka kuondoka.

Haishangazi kuwa Robert Mugabe jana alipowaambia kuwa kuna graduation alialikwa kwenda kama mgeni rasmi, akina Chiwenga wakahakikisha anakwenda.

Tusishangae, wakati taratibu za makomredi kukamilisha hesabu za Mugabe kukabidhi madaraka hazijakamilika, Mugabe anaweza pia kutokea hata kwenye sherehe ya harusi.

Kwa sasa si Mugabe anayeongoza Zimbabwe. Ni Jeshi.

Maggid Mjengwa.

0688 37 36 52