Friday, August 14, 2020
Swahili > Habari > Habari za kitaifa > Zawadi Msigala, mrithi wa Maria na Consolata.

Zawadi Msigala, mrithi wa Maria na Consolata.

Mwanafunzi mwenye ulemavu, Zawadi Msigala, ndiye anayeishi kwenye nyumba waliyokua wakiishi mapacha walioungana marehemu Maria na Consolata, kilolo mkoani Iringa . Mwanafunzi huyo alichukuliwa na shirika la Maria Consolata baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya Sekondari kutokana na ulemavu wake.

Awali, baada ya Zawadi kuhitimu darasa la saba katika shule ya msingi Tanangizi, alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya wavulana ya Songea lakini hakuweza, katika msiba wa Maria na Consolata, Zawadi alionekana akiwa mwenye sura ya huzuni juu ya baiskeli yake ya miguu mitatu pembeni ya jeneza la mapacha hao.

Mkuu wa shirika la Maria na Consolata, Jane Nugi, alisema juzi kwamba tayari wameanza kumlea Zawadi kama ilivyokuwa kwa Maria na Consolata na wanatamani kuona ndoto zake zikitimia. Alisema, Zawadi ameanza masomo ya sekondari katika shule ya Maria Consolata ” Nyota Ndogo ” waliyosoma Maria na Consolata toka kidato cha kwanza hadi cha nne.

Marehemu Maria na Consolata, mapacha walioungana.

Nugi aliongeza kuwa, ” Zawadi anaandika kwa komputa na anatumia miguu, lakini akina Maria na Consolata walikua wanaandika kwa mikono, pia Zawadi anajifunza polepole kwa hiyo anahitaji uangalizi wa hali ya juu wakati Maria na Consolata walikua wanaenda sawa na wanafunzi wengine.

Kwa upande wake Zawadi alisema, anaomba kukutana na Rais Magufuli ili amuombe atoe kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu hasa mashuleni. Zawadi amefanikiwa kuandika kitabu kwa kutumia miguu akielezea changamoto wanazokutana nazo watu wenye ulemavu.

Ndoto yake kuu ni kuwa mwanasheria,” Natamani kusoma kwa bidii nije kuwa Mwanasheria, pia natamani kuona siku moja Tanzania inaongozwa na watu wenye ulemavu ” , alisema Zawadi.