Sunday, April 21, 2019
Swahili > Afya > Wamiliki wa viwanda mikocheni watakiwa kutatua kero za uchafuzi wa mazingira ndani ya mwezi mmoja.

Wamiliki wa viwanda mikocheni watakiwa kutatua kero za uchafuzi wa mazingira ndani ya mwezi mmoja.

Wamiliki wa viwanda eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam wamepewa mwezi mmoja kutatua kero ya uchafuzi wa mazingira kwa kudhibiti utiririshaji wa majitaka unaohatarisha afya za wakazi wanaoishi kabla ya kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria.

Agizo hili lilitolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola, baada ya kutembelea viwanda vya Iron and Steel Ltd na MMI Integrated Mills Ltd vilivyopo maeneo ya Mikocheni ‘B’ kujionea uchafuzi wa mazingira.

“Nawaagiza wamiliki wa viwanda hivi wakutane na watendaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) mara moja kujadili namna ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira, utirirshaji wa maji machafu, moshi na kuutatua kero hii ya muda mrefu kwa wananchi,” alisema Lugola wakati wa ziara yake ya ghafla katika viwanda hivyo .

Maji machafu yatokayo kiwandani mitaa ya Mikocheni Jijini Dar Es Salaam-Tanzania.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa serikali za mitaa Mikocheni ‘B’ Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni, Sixbert Qamdiye, alisema wananchi wa maeneo yake kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia kero ya uchafuzi wa mazingira na maji machafu yanayotokana na viwanda hivyo licha ya ofisi yake kuchukua hatua mbalimbali kutatua kero hizo.

Naye Mratibu wa NEMC wa Mazingira Kanda ya Mashariki, Jafar Chimgege, alisema eneo la Mikocheni ‘B’ lina viwanda vingi na kusisitiza wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kushughulikia usafi wa mazingira katika maeneo hayo na kuhakikisha wamiliki wa viwanda husika wanatekeleza sheria ya mazingira ili kulinda afya za wananchi wanaoishi karibu na viwanda.