Sunday, April 21, 2019
Swahili > Elimu > Walimu walilia maslahi yao Korogwe

Walimu walilia maslahi yao Korogwe

CWT Korogwe

Na Mashaka Kibaya, Korogwe

CHAMA cha Walimu CWT wilayani Korogwe kimeahidi kuendelea kuungana na Rais Dk Magufuli kwa utendaji kazi wake ambapo mwenyekiti wa chama hicho David Nkingwa amesema wataendelea kufanya kazi kwa bidii kuunga mkono kauli mbiu ya ‘Hapa kazi tu ‘.

Licha ya kutoa ahadi hiyo Nkingwa alisema kuna haja ya serikali kuhakikisha kwamba ujenzi wa vyumba vya madarasa unaenda sambamba na uboreshaji wa madai ya walimu likiwemo suala la ujenzi wa nyumba za watumishi hao.

Mbali na kuyasema hayo, mwenyekiti huyo wa CWT amewasihi walimu kuendelea kufanya subira wakati serikali ikiendelea kushughulika na changamoto zinazowakabili walimu.

Naye katibu wa CWT wilayani humo Festo Mitimingi alisema, lengo kuu la mkutano huo ni kujadili mpango mkakati wa chama hicho, kuishauri serikali namna bora ya kuboresha maslahi ya walimu.

Walimu korogwe
Aliyesimama ni DC Korogwe, katikati mwenyekiti CWT wilaya na Festo Mitimingi katibu CWT Korogwe.

Aidha Mitimingi alisema, mkutano huo umezingatia matakwa ya kikatiba ya chama cha walimu CWT toleo namba 6 la mwaka 2004.

Mgeni rasmi kwenye mkutano huo mkuu wa wilaya ya Korogwe mhandisi Robert Gabriel alisema, baada ya vyumba vya madarasa kukamilika kinachofuata ni ujenzi wa nyumba za walimu.

Amewataka walimu kutokatishwa tamaa katika utendaji kazi wao kwa maelezo kuwa serikali imeendelea kutatua changamoto zinazowasibu walimu.

Mkuu huyo wa wilaya alipongeza utendaji kazi wa walimu licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa huku akitoa wito kwa watumishi hao kuwasiliana na ofisi ya DC kwa yale yatakayowakwaza.

Akihitimisha hotuba yake, mkuu huyo wa wilaya aliahidi kuwasiliana na wakurugenzi wa halmashauri kuangalia namna ambavyo walimu wanaweza kupewa kipaumbele pindi fursa zinapojitokeza huku akitaja mgao wa viwanja vya makazi.