Friday, August 14, 2020
Swahili > Habari > Waandishi 4 Wakamatwa Uganda

Waandishi 4 Wakamatwa Uganda

Waandishi waanchiwa

Waandishi wa habari wanne waliokuwa wamekamatwa na polisi katika mji wa Lira uliopo kaskazini mwa Uganda wameachiwa huru.

Waandishi hao walishikiliwa na polisi wakati walipokuwa wakitekeleza majukumu ya kuandika habari za waandamanaji wanaopinga kuondolewa kipengele cha ukomo wa miaka ya urais.

Isaac Otwi, mwandishi wa gazeti la Daily Monitor, Robert Kalibongo wa Unity FM, Denis Engena wa NBS na Martin Ongom, mwandishi wa Dwon Luo, gazeti la Lira mjini wote kwa pamoja walichukuliwa na polisi majira ya saa kumi na moja jioni katika barabara ya Oyite Ojok huko mjini Lira.

Baadhi ya waandamanaji hao waliwasha moto barabarani kwa kutumia matairi yaliyotumika huku wakionyesha mabango yenye ujumbe unaopinga kuondolewa kwa kipengele hicho la katiba nambari 102 (b). Hatua hiyo inaonekana kama moja wapo ya jitihada za kutaka kumuongezea rais Yoweri Museveni muda wa kuwa madarakani.

Jasper Ouni, ambae amekuwa akiripoti maandamano hayo, anasema wamekuwa wakifanya shughuli zao kama kawaida baadae polisi wa kuzuia vurugu wakatokea wakiwa katika gari sita na kuwazunguka.

Amesema polisi waliwakamata waandishi hao wa habari na kuwaingiza kwenye gari na kuwapeleka katika kituo kikuu cha polisi cha Lira.

Kwa upande wake, polisi inawatuhumu waandishi kwa kushirikiana na waandamanaji na kushindwa kutoa taarifa za mipango yao.

Wakati huo huo, polisi pia wanaripotiwa kuwatia mbaroni wanaharakati wanne kwa kushiriki maandamano hayo.