Sunday, April 21, 2019
Swahili > Biashara > Ujenzi wa Soko Korogwe Kuongezea wananchi kipato

Ujenzi wa Soko Korogwe Kuongezea wananchi kipato

Mradi wa soko Korogwe

Mashaka Kibaya Korogwe.

UJENZI wa Soko la kisasa unaendelea katika eneo la Kilole jirani na kituo kipya cha mabasi katika halmashauri ya Mji Korogwe. Mradi huo wa soko unatarajiwa kuongeza kipato kwa wananchi na halmashauri hiyo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji huo, Jumanne Shauri ametembelea eneo la ujenzi na kujionea ujenzi huo unavyoendelea.

Katika eneo hilo la ujenzi Shauri aliwataka mafundi kuongeza juhudi ili kufanikisha mradi huo haraka lengo likiwa kuharakisha maendeleo kwa wananchi Mjini humo.

Ujenzi wa soko Korogwe
Ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kuleta ukombozi kwa jamii ya wanaKorogwe ukisaidia kukuza uchumi wao na halmashauri kwa ujumla wake.

“Hapa mngeongeza kasi ‘speed’ kwa kujenga hata usiku na mchana, vifaa mnavyo vya kutosha hakuna sababu kazi kuchelewa, mkandarasi ongeza mafundi wako,” alisema Shauri.

Kwa mujibu wa Shauri ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kuleta ukombozi kwa jamii ya wanaKorogwe ukisaidia kukuza uchumi wao na halmashauri kwa ujumla wake.

Ramadhani Bakari ni mkazi wa Kata ya Bagamoyo katika halmashauri ya mji Korogwe ambapo anaelezea matumaini yake kukuza uchumi kupitia mradi huo wa Soko la kisasa.

Anasema wananchi walio wengi wakiwemo wafanyabiashara wataweza kuendesha shughuli zao kwenye soko hilo na hivyo kujiongezea kipato kitakachosaidia kuimarisha maisha ya kaya zao.

Soko Korogwe
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji Korogwe Jumanne Shauri akikagua mradi wa ujenzi soko la kisasa huko Kilole.

“Sisi kama wananchi tunafarijika na ujenzi unaoendelea, serikali inaonyesha kutujali kwa kutuimarishia miundombinu mbalimbali, kupitia soko hili tutaweza kubadili maisha “alisema.

Naye Cyprian Sadick alisema, kuna kila haja ya wananchi kuunga mkono jitihada za serikali yao ili kuweza kuharakisha maendeleo.