Sunday, January 26, 2020
Swahili > michezo > Tanzania kushiriki michuano ya Cecafa

Tanzania kushiriki michuano ya Cecafa

Soka

Baada ya miaka miwili bila kuchezwa kwa mashindano ya kuwania Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki, michuano hiyo imerejea tena msimu huu na Tanzania imethibitisha kushiriki.

Nchi wanachama Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia.

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu  Tanzania (TFF), Kidao Wilfred amethibitisha kikosi cha kwanza cha ‘Taifa Stars’ kushiriki na matarajio ya kufanya vema michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Novemba 25, 2017 hadi Desemba 9, mwaka huu.

Kidao amesema kwamba uteuzi wa timu za kwanza kwa kila nchi mwanachama wa Baraza la Mpira wa Miguu la Afrika Mashariki ni makubaliano ya viongozi wa CECAFA waliokutana kwa pamoja huko Sudan, Septemba, mwaka huu.

Kutokana na makubaliano hayo ya kuita timu za kwanza, michuano hiyo itaathiri kidogo ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuwa wachezaji wengi wanaounda kikosi hicho, wanatoka timu za VPL.

Kadhalika, Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya Chalenji kwa wanawake ikienda kutetea taji katika michuano itakayofanyika Rwanda mwezi Desemba, mwaka huu. Tarehe rasmi itatajwa baadaye.