Sunday, April 21, 2019
Swahili > Maoni > Shambulizi la Texas na undumilakuwili vita dhidi ya ugaidi

Shambulizi la Texas na undumilakuwili vita dhidi ya ugaidi

Shambulizi Texas

Na Yusufu Lulungu

Kwa mara nyingine, tena ndani ya kipindi kifupi Marekani imetikiswa na shambulizi la kuogofya na lisilo na huruma. Ni shambulizi la kwenye kanisa jijini Texas ambalo limechukua roho za waamini wa Kikristo 26 na kuwaacha wengine na majeruhi

Shambulizi hilo limefanywa na Devin Patrick Kelley, mzungu, mpagani, raia wa Marekani ambaye anatajwa kuwa aliwahi kuwa mwanajeshi katika jeshi la anga nchini humo.

Pia, inatajwa kuwa aliwahi kufungwa na kufukuzwa kazi kwa matendo yasiyoridhisha ikiwemo kugombana na familia yake.

Shambulizi hili limejiri ikiwa haijapita wiki moja tangu kutokea kwa shambulizi la New York ambalo lilikatisha uhai wa watu 8.

Pia shambulizi hilo linatokea takribani mwezi mmoja tangu lile la Las Vegas ambalo lilikatisha pumzi ya watu 58 na kujeruhi wengine.

Hisia za Trump

 Akiliongelea shambulizi hilo la Texas, Rais Donald Trump amesema ni tukio la uovu na kwamba mshambuliaji alikuwa na matatizo ya akili. Kwa lugha rahisi ni “chizi”.

Hisia za Rais Trump juu ya tukio hilo zinaashiria vitu viwili. Mosi, kukwepa hoja za mjadala wa udhibiti wa umiliki wa silaha nchini humo. Suala hilo limepamba moto sana kwa sasa kutokana na kukithiri kwa mashambulizi nchini humo.

Raia wengi nchini humo na hata baadhi ya viongozi wa kisiasa hususani wa Chama cha Democratic wanataka silaha zidhibitiwe.

Pili, “utetezi” wa Trump unatazamwa kama njia ya Rais huyo kukwepa mjadala wa ugaidi, kwa kuwa mshambuliaji wa Texas ni mzungu na ni raia wa Marekani.

Katika shambulizi hilo, katika waliouawa 26, nane wanatoka katika familia moja. Kimsingi, Kelley hana tofauti na washambuliaji wengine ambao huitwa magaidi.

Kama suala ni chuki za kidini, hata Kelley pia anatajwa kuwa alikuwa na chuki dhidi ya Wakristo na ameripotiwa alikuwa akiubeza Ukristo kupitia mitandao ya kijamii, suiku chache kabla ya kufanya tukio hilo la kinyama.

Pia kusema ni “chizi, Trump anamuondoa Kelley haraka kwenye hoja zinazoweza kuibuka hapo baadaye kuwa kulikuwa na msukumo wa kundi fulani la kigaidi kwa mshambuliaji huyo.

Hivyo, hata kama kundi la IS lingeweza kuchomoza na kusema Kelley ni mtu wao, hoja hiyo ingekosa nguvu sana kwa kuwa dunia imeshaambiwa mshambuliaji huyo ni “mwehu.”

Ugaidi sio ugaidi?

 Tukija kwenye maana ya ugaidi, kama nilivyoonesha wiki kadhaa zilizopita wakati nikijadili tukio la Las Vegas, tafsiri ya neno ugaidi ina utata.

Utata unakuja kwa sababu inaonekana kuna undumilakuwili katika kuainisha matukio haya, lipi ni ugaidi, lipi si ugaidi?

Mfano hai ni kuwa, wakati tukio la New York lililofanywa na Muislamu lilisababisha vifo vya watu 8 limeitwa ni ugaidi, lile la Las Vegas na Texas yaliyosababisha vifo 58 na 26 ambayo yamefanywa na wasio Waislamu yanaonekana sio ugaidi.

Tunaweza tukarejea kuutazama utata huo kupitia tafsiri za ugaidi ambazo zinatolewa na mamlaka za Marekani.

Shirika la Upelelezi wa Ndani la Marekani (FBI) limetaja ugaidi kuwa ni: “The unlawful use of force or violence against persons or property to intimidate or coerce a government, the civilian population, or any segment thereof in furtherance of political or social objectives.”

Kwa tafsiri isiyo rasmi: “Ugaidi ni kitendo cha kutumiaji  nguvu au vurugu kinyume cha sheria dhidi ya watu au mali ili kutoa vitisho au kuilazimisha serikali, raia au kundi lolote ili kutimiza malengo ya kisiasa au kijamii.””

Lakini kwa mujibu wa tafsiri ya jimbo la Nevada, Marekani humo humo inatafsiri Ugaidi kama: “”The use or attempted use of sabotage, coercion or violence which is intended to cause great bodily harm or death to the general population.”

Kwa tafsiri isiyo rasmi ugaidi ni: “Matumizi au kujaribu kutumia hujuma, nguvu au vurugu ambazo dhamira yake ni kudhuru mwili au kusababisha kifo kwa watu wengi.”

Nikianza na tafsiri ya pili ya Nevada, yenyewe haina utata, Kelley moja kwa moja anaingia kwenye kundi la magaidi, kwani kaua, kajeruhi  kaleta hofu kwa watu wengi nchini humo.

Kwa upande wa tafsiri ya kwanza iliyojikita juu ya  nia (intent)  kama kigezo cha tukio kuitwa la kigaidi, hapa leo naomba niiache dhamira ya kisiasa, tuje kwenye dhamira ya kijamii kama ilivyo kwenye hiyo tafsiri.

Kwenye tafsiri hiyo, kuna suala la dhamira ya kijamii (social objectives), kwamba tukio la kigaidi linaweza kuwa kwenye mtazamo wa kijamii.

Na kwa tafsiri ya kawaida  matukio ya kijamii yanaweza kuwa, ubaguzi wa rangi, chuki za aina mbali mbali kama za kidini, kikabila, kikoo na hata kimadhehebu.

Mpaka sasa dhamira ya Kelley ya kufanya shambulizi, tumeambiwa bado inachunguzwa, lakini kama tulivyogusia, Kelley alikuwa akituma ujumbe wa kukejeli  Ukristo katika mitandao ya kijamii

Pia, ukiangalia hisia za watu wengi wa Marekani wanalitazama tukio la Texas kama lililojaa chuki, visasi na uovu. Huenda dhana hiyo inajengwa kufuatia mshambuliaji huyo kuua watu nane wa familia moja.

Mathalani, Rais  mstaafu Obama kwenye akaunti yake ya Twitter aliandika: “Tunahuzunika pamoja na familia zilizokumbwa na mkasa wa Sutherland Springs, zilizojeruhiwa na kitendo cha CHUKI…”

Lakini hata Trump mwenyewe amesema ni tukio la uovu bila kusema ni uovu wa aina gani. Kwa mtazamo wa kawaida tu hata ugaidi nao ni uovu pia.

Matamshi ya watu kadhaa kusema shambulizi la Texas ni tukio la chuki, linaingiza tukio hilo kwenye ugaidi kwa mujibu wa tafsiri ya FBI.

Hata hivyo wenye mamlaka wamegoma” kuita tukio hilo kuwa ni ugaidi na kuishia kusema ni uovu tu.

Kwa ujumla, tukio la Texas linazidi kutoa picha kuwa ugaidi  katika uhalisia ni dhana iliyofungamanishwa na itikadi ya kundi fulani, hususan Waislamu; maana matukio mengi ya aina moja yanatokea ila hukumu yake inakuwa tofauti.

Na pia matukio haya yanazidi kuonesha ni kwa namna gani tafsiri ya akina Trump na wenzake ni kuwa ugaidi ni Uislamu na Uislamu ndio ugaidi.