Friday, August 14, 2020
Swahili > Habari > Habari za kimataifa > Rwanda kupeleka Askari wa kike kulinda amani Sudan

Rwanda kupeleka Askari wa kike kulinda amani Sudan

Rwanda inatarajia kupeleka nchini Sudan Kusini walinda amani wa kike pekee kwa ajili ya vikosi vya Umoja wa Mataifa. Askari wa kike wa Rwanda wanatarajiwa kuwa wa kwanza wa jinsia hiyo duniani kuwahi kupelekwa kulinda amani katika nchi nyingine.

Wanatarajiwa kuondoka nchini hivi karibuni, kwenda kutimiza majukumu yote yanayopaswa kufanywa na vikao vya walinda amani wa umoja wa mataifa.

Kwa mujibu wa Naibu Inspekta Jenerali wa polisi, Dan Munyuza, taratibu zote zimeshakamilika na amewataka walioteuliwa wakafanye kazi yao kwa uadilifu hata kama watakumbana na mazingira magumu ya kikazi.

Dan Munyuza, Naibu Inspekta Jenerali wa polisi – Rwnda.

Mwaka 2009, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alizindua kampeni ya kuongeza idadi ya walinda amani wa kike kutoka asilimia 10 hadi 20 kufikia mwaka 2014. Hata hivyo, idadi hiyo haikufikiwa na nchi nyingi.

Rwanda kwa mara ya kwanza ilituma walinda amani wake Sudan Kusini mwaka 2015 na ni moja ya nchi zenye idadi kubwa ya walinda amani wa umoja wa mataifa nchini humo.