Friday, August 14, 2020
Swahili > Habari > Habari za kimataifa > Maziwa makuu na mkutano kuhusu makosa ya jinai,Dar Es Salaam-Tanzania.

Maziwa makuu na mkutano kuhusu makosa ya jinai,Dar Es Salaam-Tanzania.

Mkutano wa ngazi ya juu wa Jumuia ya nchi za Maziwa Makuu unaohusu ushirikiano katika masuala ya makosa ya jinai, umeanza hii leo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ambapo wawakilishi kutoka nchi mbali mbali wanahudhuria.

Lengo kuu la mkutano huo ni pamoja na kubadilishana taarifa za kesi mbalimbali na kubadilishana watuhumiwa wanaokamatwa katika nchi nyingine.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili, Balozi Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya nchi za Maziwa Makuu Said Djinnit amesema kuwa viongozi wa eneo la Maziwa Makuu wameazimia kupambana na suala la wahalifu kuepuka adhabu, hivyo kuimarisha ushirikiano wa kimahakama kama njia moja wapo ya kupunguza uhalifu katika eneo hilo.

“Mbali na jitihada zinazofanyika kitaifa, bado kuna wahalifu ambao hawajakamatwa. ”Kwa masikitiko hakuna ushirikiano wa kutosha wa kimahakama baina ya nchi wanachama, matokeo yake, hawa watuhumiwa bado wako huru,” amesema balozi Djinnit.

Wajumbe wa mkutano wa jumuia ya nchi za maziwa makuu.

Mkutano huo unatarajiwa kutoka maazimio ya namna ya kutekeleza mikataba na makubaliano yaliyopo ya ushirikiano katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Mkutano huu ni wa pili kufanyika, wa kwanza ulifanyika mwezi Novemba mwaka jana mjini Khartoum, nchini Sudan.