Friday, August 14, 2020
Swahili > michezo > Matola, nimepewa ofa nyingi na vilabu vya VPL.

Matola, nimepewa ofa nyingi na vilabu vya VPL.

Baada ya kuisaidia Lipuli FC kuonyesha soka la kuvutia na lenye ushindani katika msimu wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara uliomalizika hivi karibuni, kocha wa timu hiyo ya Iringa, Selemani Matola, amesema kuwa, klabu mbalimbali zimempa ofa ya kutakwa kumwajiri.

Matola ambaye yuko jijini Dar es Salaam kwa mapumziko alisema kuwa ana ofa zaidi ya nne mezani kutoka kwa klabu za Ligi Kuu ikiwamo Lipuli ambayo anaifundisha.

Hata hivyo Matola alikataa kuzitaja klabu ambazo zimeomba kufanya mazungumzo naye na anasema kuwa amefarijika kuona uwezo wake umekubalika na unaheshimiwa.

Kikosi cha timu ya Lipuli FC – VPL

“Nimepokea ofa mbalimbali kutoka kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu, hali hii imenifariji, watu wameanza kuona uwezo wangu na kutuheshimu makocha wazawa, ila ninaipa nafasi ya kwanza Lipuli, pale ni rahisi kuendelea kuliko klabu nyingine mpya itanilazimu kuanza upya,” alisema kiungo na nahodha huyo wa zamani wa Simba.

Matola aliisadia Lipuli kumaliza katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 38 baada ya kushinda mechi tisa, sare 11 na kufungwa michezo 10.