Sunday, April 21, 2019
Swahili > Utalii > Maajabu ya Bonde la Ngorongoro

Maajabu ya Bonde la Ngorongoro

Utalii Ngorongoro

HIFADHI ya Wanyama Ngorongoro imegubikwa na simulizi za mambo mengi ya kihistoria yenye kusisimua huku jambo kubwa likiwa ni uwepo wa bonde lenye kina kirefu lililogundulika zaidi ya miaka milioni moja iliyopita.

Bonde hili si jingine ila ni lile lenye kufahamika kwa jina la Ngorongoro ‘Ngorongoro Crater’ ambalo wataalamu wanaeleza kuwa uwepo wake ni matokeo ya Volkano iliyotengeneza shimo lenye urefu wa takribani mita 600.

Umaarufu wa Ngorongoro Crater unatokana na uwepo wa vivutio vingi vya utalii ambavyo havipatikani eneo jingine duniani jambo ambalo limedhihirishwa na shirika la kimataifa la UNESCO baada ya kulifanya eneo hilo kuwa urithi wa Dunia ‘The World Heritage Site.’

Dk Freddy Manongi ni mhifadhi mkuu wa hifadhi ya Wanyama Ngorongoro ambaye anaeleza kuwa, umaarufu wa bonde hilo unatokana na umbile lake ambalo halikuvunjika hivyo kutengeneza taswira yenye kustaajabisha duniani.

“Si kwamba hakuna mabonde mengine yapo ila muonekano wake siyo kama huu wa Ngorongoro, hili halikuvunjika na ni kubwa sana,” anasema Dk Manongi.

Ujangili Tembo
Kuhusu mkakati wa kuzuia vitendo vya ujangili hususani kuuawa kwa wanyamapori hasa Tembo, Dk Manongi anasema kwa sasa hali ni shwari baada ya elimu kutolewa kwa watu wanayoishi pembezoni mwa hifadhi ya Ngorongoro.

Anaongeza kusema tangu zamani watu wa kabila la Wamasai waliishi ndani ya bonde hilo ingawaje mwaka 1959 waligawanywa wengine wakihamishiwa pori tengefu linalofahamika kwa jina la Loliondo.

Wenyeji zaidi ya 4,000 wakiishi hapo wakiwa wamechanganyikana na wanyamapori jambo ambalo limeonekana kuwa siyo kawaida na hivyo kuwa moja ya kivutio cha utalii.

Anayataja makabila yanayoendelea kuishi ndani ya bonde hilo la Ngorongoro kuwa ni Wamasai ambao kiasili ni wafugaji ng’ombe, watatoga na wahadzabe ambao wameruhusiwa kuishi humo kwa mujibu wa sheria.

Ni wapi hifadhi ya Ngorongoro imetoka?

Dk Manongi anasema mnamo mwaka 1940 serikali ya Kiingereza kwa makusudi kabisa ilianzisha ‘game reserve ‘ wakati huo Ngorongoro ikiwa sehemu ya Serengeti kulikoonekana kuwa sehemu nzuri kwa utalii wa picha.

Dk Manongi anasema kuwa, hapo awali Ngorongoro ilikuwa kitengo chini ya idara ya wanyama pori hadi mwaka 1981 ilipoamriwa kupewa sifa kuwa ‘man and biosphere reserve ‘ hivyo watu kuanza kushirikishwa utunzaji wanyama pori.

Ili kutokujitokeza kwa suala la uharibifu wa mazingira, wenyeji ambao walikuwa wakiishi kwa muda mrefu kwenye eneo hilo walitakiwa kutoendesha shughuli nyingine yeyote isipokuwa ile ya ufugaji.

Tangu hapo jamii iliweza kushirikishwa kikamilifu kwa uhifadhi wa wanyamapori na wenyeji walioishi ndani ya eneo hilo wakatengezewa mazingira ya kuwa sehemu ya kivutio cha suala la utalii.

Mashaka Kibaya
Mwandishi wa makala hii Mashaka Kibaya akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wenzake katika Bonde la Ngorongoro.

Mbali na hayo bonde la Ngorongoro ni muhimu kwa upatikanaji mali kale, eneo ambalo pia wanyama aina ya nyumbu wamekuwa wakizaliana kwa wingi kipindi vya mvua za masika kuliko maeneo mengine duniani kote.

Kwa mujibu wa Dk Manongi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro Wanyama kama Tembo, Simba, Nyati, Faru, Chui na wanyama wengine ni rahisi kuonekana wakiwa katika mazingira yao ya asili.

Akizungumzia zaidi umuhimu wa bonde la Ngorongoro, Dk Manongi anasema baada ya kugundulika kuwa kivutio kikuu cha utalii unaosaidia ukuaji wa uchumi kanda ya kaskazini na hata ngazi ya Taifa maazimio kadhaa yamefikiwa.

Katika maazimio hayo yalilenga kuimarisha uhifadhi wa Ngorongoro na hivyo kutokana na umuhimu wake Duniani, shirika la kimataifa la UNESCO limekuwa mbia mkubwa wa kuhakikisha ustawi wa eneo hilo unakuwa wenye maslahi mapana kwa wanadamu.

Mambo mengine yaliyoipa umaarufu Ngorongoro ni uwepo wa masalia ya unyayo wa binadamu zaidi ya miaka milioni mbili.Zinapatikana huko Laitoli ambapo zinazothibitisha binadamu alivyoanza kutembea kwa miguu miwili.

Kwa kuingia mikataba na UNESCO manufaa makubwa yameanza kuonekana ikiwa ni pamoja na ongezeko la watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani wakiwemo watu waliyo maarufu.

Ili tija zaidi kuweza kupatikana kupitia hifadhi hii ya Ngorongoro inayopata umaarufu mkubwa kupitia bonde lililopo, UNESCO mwaka 1979 na ilipofika 1981 walipendekeza hifadhi hiyo kuwa urithi wa Dunia ikaongezeka kuwa man and biosphere reserve(watu na wanyama).

Mhifadhi Mkuu Ngorongoro.
Dk Freddy Manongi ni mhifadhi mkuu wa hifadhi ya Wanyama Ngorongoro.

Wakati hayo yote yakifanyika tayari mwaka 1974 sheria ya Wanyama pori ilianzisha mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kuruhusu shughuli za uhifadhi wanyama pori na utalii wa picha kuendelea kufanyika.

Hata hivyo hifadhi hii ya Ngorongoro mwaka 2010 iliwekewa mikakati zaidi na mchakato umefanyika ili eneo hilo kuweza kuwa la kijiolojia utaratibu ambao tayari umewasilishwa UNESCO.

Kuhusu mkakati wa kuzuia vitendo vya ujangili hususani kuuawa kwa wanyamapori hasa Tembo, Dk Manongi anasema kwa sasa hali ni shwari baada ya elimu kutolewa kwa watu wanayoishi pembezoni mwa hifadhi ya Ngorongoro.

Jitihada nyingine ni kuimarisha ulinzi kwa Tembo kupitia mtandao wa sattelite ambapo wanyama hao wamekuwa wakifungwa kifaa maalum kinachoitwa kola lengo likiwa kurahisisha mawasiliano juu ya mahali walipo.

Akizungumzia zaidi kitengo maalum kinachohusika na utoaji elimu kwa umma Dk Manongi anasema,kimeendelea kuhusika kuelimisha jamii kufanya shughuli mbadala pasipo kutegemea uwindaji wa wanyamapori.

Hata hivyo anatanabaisha kwamba hapo awali hali ulikuwa mbaya kutokana na majirani kuhusika kwa namna moja ama nyingine wakishirikiana na wageni kwenye vitendo vya ujangili viivyokuwa vikichangiwa na uwepo wa masoko.

Anasema, ujangili ambao ulikuwa ukiwasumbua ni ule wa baadhi ya watu wasio wazalendo kutumia sumu ambayo walikuwa wakiweka kwenye maboga ili kuua Tembo kwa lengo la kupata pembe au meno ili kuyauza.

Kupitia dawati mahususi la elimu, mtandao wa ujangili umeweza kudhibitiwa mpaka kufikia ngazi za chini ingawaje Dk Manongi anasisitiza elimu inahitajika zaidi kule ambako wamekuwa wakihisi bidhaa zitokanazo na wanyama hasa Tembo zinahitajika.

Dk Manongi anasema, kwa vile masoko mengi ya bidhaa hizo yamegundulika kuwa nje ya nchi,vikao vya kimataifa vimekiwa vikifanyika kupiga marufuku jambo hilo huku akisisitiza kusema kuwa kamwe uzi hautalegezwa katika kuwashughulikia watu walio majangili.

Dk Manongi anahitimisha makala haya kwa kuwaomba Watanzania na wadau wa sekta ya habari kutumia nguvu zao zote katika kulinda urithi huu wa Dunia inapatikana hifadhi ya Ngorongoro.