Sunday, April 21, 2019
Swahili > Elimu > Korogwe yaja na Mradi wa Jitambue Mwanamke

Korogwe yaja na Mradi wa Jitambue Mwanamke

Mimba na ndoa za utotoni

JITAMBUE Mwanamke ni taasisi binafsi yenye makao yake makuu huko kata ya Old Korogwe katika halmashauri ya Mji Korogwe huku malengo yake makuu yakiwa ni kupinga na kukemea mimba na ndoa za utotoni.

Katika utekelezaji wa majukumu yake asasi hii inaundwa na wanawake ambao kwa umoja wao wamedhamiria kuunganisha nguvu zao ili kutetea maslahi yao hatua itakayo wasaidia kuwawezesha kufikia ndoto zao.

Ikiwa ni miezi takribani sita (6) tangu kwa asasi hiyo kuanza kutekeleza rasmi majukumu yake Jitambue Mwanamke imefanikiwa kujitanua kwenye mikoani kadhaa nchini lengo ni kuifikia sehemu kubwa ya jamii.

Mkurugenzi mtendaji wa asasi hiyo Mwanaidi Awadhi Kipingu anasema, kilichowasukuma kuunda chombo hicho ni baada ya kugundulika idadi kubwa ya watoto wa kike wanakatiza masomo kwa kuwa wajawazito.

Ndoa za utotoni
Elimu ambayo wamekuwa wakiitoa ni ile ya kujitambua ambapo wahusika wamekuwa wakitengenezewa mazingira ya kujitambua ambapo wanafunzi wanaohitajika shule za msingi na sekondari wanahusishwa.

Anasema changamoto hiyo kwa watoto wa kike kwa kiasi kikubwa inachangiwa kushamiri kwa mfumo dume ambao umekuwa ukisababisha kuzorotesha maendeleo ya wanawake na Taifa kwa ujumla wake.

Kuhusu shughuli ambazo wamekuwa wakizifanya kupitia asasi hiyo, Kipingu anasema ni pamoja na utoaji elimu kwa jamii hususani watoto wa kike chini ya miaka 16 waliopo shule na hata mitaani na vijiji mbalimbali.

Elimu ambayo wamekuwa wakiitoa ni ile ya kujitambua ambapo wahusika wamekuwa wakitengenezewa mazingira ya kujitambua ambapo wanafunzi wanaohitajika shule za msingi na sekondari wanahusishwa.

Mbali na elimu hiyo kwa wanafunzi lakini pia watoto wa kike waliopo mitaani wamekuwa wakifundishwa masomo ya ujasiriamali kama vile utengenezaji batiki, sabuni na ufugaji wa kuku ili kujikwamua.

Lengo kuu la elimu hii ya ujasiriamali ni kuwawezesha mabinti hao kuondokana na mazingira tegemezi hatua ambayo imekuwa ikichangia kujiingiza kwenye tamaa za kimaisha hivyo kujikuta wakiingia mtegoni.

Kwa mujibu wa Kipingu asasi hiyo inaundwa na wanawake wa taaluma tofauti, ila na hutumia nafasi zao kuleta ukombozi kwa jamii ya watoto wa kike nchini Tanzania lengo likiwa kuongeza uwezo wa kada hiyo.

Amewataja baadhi ya wanataaluma wanaounda asasi hiyo kuwa ni pamoja na mataibu, walimu na hata wataalam wa kada nyingine ambao kwa umoja wao wamekuwa wakifanya kila liwezekanalo kuwakwamua wanawake.

Kuhusu mafanikio yaliyoanza kupatikana katika kipindi hicho kifupi tangu taasisi kuanzishwa, Kipingu anasema amefanikiwa kuanzisha vilabu huku wakipata mabalozi kupambana na changamoto dhidi ya watoto wa kike.

Akizungumzia zaidi changamoto wanazokabiliana nazo katika utendaji kazi wao, Kipingu anasema kwamba kuna baadhi ya familia zimekuwa na tabia ya kuwaficha watuhumiwa wa vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto.

Pia amesema lipo tatizo la kisheria ambapo sheria ya ndoa ya mwaka 1971 imekuwa ikichangia kutoa mwanya kwa watoto wa klike kuanzia umri wa miaka 15 kupata ruksa kuolewa jambo analolieleza kuwa halifai.

Anafafanua kwa kusema sheria hiyo inaelekeza kuwa kwa ridhaa ya wazazi mtoto wa kike atakapotimiza umri wa miaka 15 anaweza kuolewa ambapo Kipingu anashauri kwa eneo hilo kurekebishwa.

Pia anataja mazingira ambayo yameonekana kuwa kikwazo kwa watoto wa kike kutimiza ndoto zao kutokana na umbali mrefu kutoka kwenye nyumba zao hadi shule huku njiani wakikumbana na changamoto kadhaa.

Aidha Kipingu anasema, kwenye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto ambapo hivi sasa wamekuwa wakihaha huku na kule kusaka eneo la kutosha kuendeshea shughuli zao.

Mbali na suala la eneo Kipingi anaelezea changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa ufadhili ambapo shughuli zote tangu asasi yao kuanza kazi rasmi utendaji mzima umekuwa ukitegemea nguvu zao.

“Kiukweli tunaweza kupambana kwa vile tumedhamiria kuwakomboa wanawake wenzetu ila ni ngumu kwa vile hatuna ufadhili wa aina yeyote ile “anasema Kipingu akielezea ukata ambao umekuwa ukiwakumba.

Licha ya changamoto hizo Kipingu anasema, kamwe hazijawakatisha tamaa kuendelea na shughuli yao zinazolenga kumkwamua mtoto wa kike akisema wamejidhatiti kuifikisha asasi yao kwenye ngazi za kimataifa.

Anasema ili kufikia hatua hiyo kwa umoja wao wa kuhakikisha kuwa wanawake wanazikifikia njia kuu za uchumi kwa kumiliki mali hususani kwenye umiliki ardhi sanjari na kukuza mahusiano na asasi nyingine.

Jitambue mwanamke mtandao wake wa utoaji huduma umefanikiwa katika mikoa ya Shinyanga, Mara, Dar es salaam na Iringa kote huko kukiwa na mabalozi wanaosaka ukombozi wa watoto wa kike.

Jitihada hizi zinakuja wakati ambapo, rais John Pombe Magufuli amepiga marufuku kwa watoto wa kike wanaopata mimba wakiwa mashuleni kuendelea na masomo. Hata hivyo, kauli yake hiyo, imepokelewa kwa hisia tofauti huku wengine wakihisi, inaweza kurudisha nyuma jitihada ambazo tayari zimefikiwa katika kumwezesha mtoto wa kike.