Friday, August 14, 2020
Swahili > Habari > Habari za kimataifa > habari > Kim na Trump, uso kwa uso Singapore.

Kim na Trump, uso kwa uso Singapore.

Rais wa Marekani Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un wamewasili nchini Singapore kwa ajili ya mkutano wao unaoelezwa kuwa wa kihistoria. Trump, aliwasili saa chache tu baada ya Kim kuwasili na ujumbe wake.

Mkutano wao ambao ni wa kwanza utafanyika siku ya Jumanne katika kisiwa cha Sentosa. Marekani ina matumaini kuwa kukutana huko kutakuwa mwanzo wa mchakato ambao hatimaye itashuhudiwa Kim akiachana na mpango wake wa silaha za nyuklia.

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini.

Uhusiano wa viongozi hawa wawili umepitia kwenye milima na mbonde kwa kipindi cha miezi 18 iliyopita, wakirushiana matusi na kutishiana vita kabla ya wawili hao kukutana. Mwaka wa kwanza wa Trump katika kiti cha urais ulianza kwa mvutano mkubwa na kurushiana maneno huku Kim naye akiendeleza majaribio ya silaha za nyuklia na kukiuka ilani ya kimataifa.

Rais wa Marekani aliapa kupambana ikiwa Pyongyang itaendelea kuitishia Marekani, wote wakipeana majina ya kukebehi. Korea Kaskazini iliendelea kukaidi na kufanya jaribio la nyuklia la sita mwezi Septemba mwaka 2017. Baadae Kim alitangaza kuwa nchi yake imefanikiwa mpango wake wa kua taifa la nyuklia, likiwa na silaha zinazoweza kuifikia Marekani.

Donald Trump,Rais wa Marekani.

Lakini mwanzoni mwa mwaka 2018, Korea Kaskazini ilianza kuboresha mahusiano na Korea Kusini kwa kupeleka timu na ujumbe kwenye michuano ya Olimpiki mjini Pyeongchang. Mwezi Machi, Donald Trump aliushangaza ulimwengu kwa kukubali mwaliko kutoka kwa Kim wa kukutana ana kwa ana.

Singapore ni nchi ya tatu ambayo Kim Jong-un ameitembelea tangu alipokuwa Kiongozi mwaka 2011. safari yake ya kwanza ilikuwa nchini China mwezi Machi na mwezi Aprili akawa kiongozi wa kwanza wa Korea Kaskazini kutembelea Korea Kusini ambapo alikutana na Moon Jae-in.