Sunday, April 21, 2019
Swahili > Habari > Kenya yaweka mikakati kuzuia Ebola

Kenya yaweka mikakati kuzuia Ebola

Kenya

Babu Zingo

Serikali ya Kenya imesema itaanza kuwachunguza watu wote wanaoingia nchini humo kutoka mataifa ya nje kufuatia kuzuka tena kwa ugonjwa hatari wa Ebola katika jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Waziri wa afya nchini Kenya Sicily Kariuki kupitia taarifa kwa vyombo vya habari amesema kulingana na masharti ya kimataifa ya afya, Kenya imeanza kukagua watu wote wanaoingia nchini humo kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta uliopo mjini Nairobi na pia mipaka ya Busia na Balaba.

Waziri Sicily ameongeza kuwa wameweka maafisa wa afya katika maeneo hayo wakiwa na vifaa vya kubaini hali ya joto mwilini, kwa lengo la kutambua wale ambao wana viwango vya juu vya joto kuliko kawaida na ambao huenda wana Ebola ili kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini Kenya.

Aidha wizara ya afya pia imebuni baraza la kitaifa la afya ambalo jukumu lake kuu ni kuweka mikakati ya kuzuia Ebola kuingia Kenya.

Hata hivyo waziri huyo amewashauri wakenya kutoingiwa hofu kwani Kenya ina uwezo wa kutambua Ebola ili kuzuia usiingie nchini.

Mbali na Kenya, Nigeria pia imetangaza kuchukua hatua za dharura za kuzuia Ebola kuingia nchini humo.