Wednesday, August 21, 2019
Swahili > Habari > Kadinali anaekabiliwa na unyanyasaji kingono kupanda kizimbani Machi mwakani

Kadinali anaekabiliwa na unyanyasaji kingono kupanda kizimbani Machi mwakani

Kadinali wa kanisa katoliki George Pell anaekabiliwa na mashitaka ya unyanyasaji kingono kwa watoto wadogo, atafikishwa tena mahakamani mwezi machi mwakani ili kujitetea juu ya madai hayo.

Polisi nchini Australia iliamua kumshitaki Kardinali huyo mapema mwaka huu, baada ya kupata ushauri kutoka kwa viongozi wa mashitaka mwezi mei mwaka huu.

Hata hivyo Kardinali huyo mwenye miaka 76 sasa, amekuwa akikana shutuma hizo akisema zinafanywa makusudi ili kumchafua lakini amependekeza uchunguzi zaidi ufanyike juu ya suala hilo.

Mwaka 2016, Shirika la Utangazaji la Australia (ABC) lilitangaza taarifa za wanaume wawili, waliodai kunyanyaswa kingono na Kardinali huyo miaka  ya 1970, wakati walipokuwa watoto wadogo.

Mwanasheria wake anasema kuwa kadinali huyo ataendelea kukana tuhuma hizo.

Kadinali huyo ambae alifunguliwa mashitaka mwezi juni mwaka huu, hapo jana Ijumaa alijipeleka mwenyewe kwenye mahakama ya Melbourne kwa ajili ya masuala ya kiutawala.

Kwa taarifa zilioko mahakamani hapo ni kwamba watu takribani 50 watatoa ushahidi hapo mwezi machi.

Kesi hiyo inatajwa kuwa itasikilizwa kwa muda wa wiki nne ambapo mahakimu wataangalia kama kuna ushahidi wa kutosha wa kesi hiyo kwenda mahakama za juu zaidi.

Hata hivyo maelezo ya kutosha bado hayajatolewa juu ya shutumu zinazomkabili kadinali Pell.

 Chanzo: BBC