Friday, August 14, 2020
Swahili > Habari > Hali Ya Tundu Lissu Inazidi Kuimarika

Hali Ya Tundu Lissu Inazidi Kuimarika

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa hali ya mbunge wake Tundu Lissu imeimarika tofauti na hapo awali. Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

Itakumbukwa kuwa ni wiki takribani mbili zimepita tangu Lissu ambae pia ni rais wa Chama cha Mawakili nchini kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana huko mjini Dodoma na baadaye kuhamishiwa hospitali ya Agha Khan iliyopo jijini Nairobi.

Ambapo kwa siku zote hizo kumekuwepo na taarifa mbalimbali kuhusu maendeleo ya afya ya Lissu ambapo mwenyekiti wa chama hicho amesema kuwa kimewataka watanzania kupuuzia taarifa mbalimbali zinazoenezwa mitandaoni kuhusiana na hali ya Tundu Lissu ambazo zinatolewa na vyanzo visivyo rasmi.

Mbali na kutoa wito huo pia amewataka waandishi wa habari kuzingatia kanuni za uandishi wa habari na si kuandika mambo kwa ushabiki na pasipo kuwa na uhakikia wa habari hizo.

“Niwatahadharishe sana wanahabari kuchukua habari za udaku na kuzirusha bila kuwa na official statement ya chama tafadhalini sana, mnafikiri mnamsaidia Lissu lakini mnaimuiza familia yake..

Gharama za Matibabu

Akitaja gharama mbalimbali za matibabu zilizotumika hadi sasa kumtibu Lissu amesema kuwa anawashukru wananchi waliojitolea kuchanga pesa kwa ajili ya matibabu ya Lissu.

Kuwa hadi sasa wamepokea zaidi ya kiasi cha shilingi milion 174 kutoka vyanzo mbalimbali vikiwemo wanachama, wabunge wa chadema na wengine na marafiki wenye mapenzi mema na Tundu Lissu.

Lakini pia anasikitishwa na kutofika kwa pesa zilizochangwa kutoka kwa posho za wabunge kiasi cha Milioni 43 pesa za kitanzania. Pia kushangazwa na kauli iliyotolewa na serikali kupitia waziri wa Afya Ummmy Mwalimu juu ya serikali kumtibu Tundu Lissu katika nchi yoyote ile.

Mbowe amesema kuwa ni jukumu la Bunge kumtibu mbunge na ni stahiki yake na kusema kuwa Bunge lilikataa kumtibu mbunge huyo.

Kwa sasa wanahitaji barua ya kuomba kumtibu Lissu jambo ambalo Mbowe amekataa na kusema kuwa kama wanataka kumtibu wasiweke masharti katika matibabu ya Lissu.

“Kutibiwa kwa wabunge na serikali ni stahiki, na wabunge wengi wameugua kwa nyakati tofauti wametibiwa na serikali na wala familia hazikupeleka maombi. Ingekuwa ni Mke au mtoto wa Lissu ndio anatibiwa kwa kofia ya baba yake, baba yake angeandika barua kuomba mwanae au mke wake atibiwe.

Lakini huyu ni mbunge ameshambuliwa akiwa Dodoma kazini, Mbowe niandike maombi wakati spika tulikuwa naye hospitalini. Walikataa kufanya jukumu ili wakitaka kulirudia, wasilirudie kwa masharti maana ni jukumu lao kulifanya”.

Mbowe pia amelaani vitendo mbalimbali vinavyoendelea kufanya na jeshi la polisi hasa vya kamata kamata ya watu wanaojitolea kutoa damu kwa ajili ya wananchi wa Tanzania. Ambapo amesema kuwa jambo hilo linachafua sura ya Tanzania kimataifa na halina mashiko yoyote yale.

Uchunguzi wa tukio

Mbowe amesisitiza kuwa hawana imani na vyombo vya kiuchunguzi vya Tanzania, kwani kama chama kinaamini kuwa vyombo vya ulinzi vya Tanzania vilihusika katika Tukio la shambulizi dhidi ya Lissu. Na hivyo kuiomba serikali ya Tanzania kuridhia maombi ya chama hicho kuleta vyombo vya kiuchunguzi vya kimataifa kama vya FBI, Scoltland Yard, Israel na vingine kutoka mataifa mengine. Ili vije vifanye uchunguzi dhidi ya tukio ili kuondoa lawama zilizopo dhidi ya kutokuaminiana dhidi ya CHADEMA na vyombo vya ulinzi.