Friday, August 14, 2020
Swahili > Habari > Balozi Seif: Mke wangu aliuza bangili ili niwe mbunge

Balozi Seif: Mke wangu aliuza bangili ili niwe mbunge

Balozi Seif Ali Idd.

Na Mwandishi wetu.

Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ), Balozi Seif Ali Idd amesema kuwa wakati anagombea ubunge  kwa mara ya kwanza mwaka 2005 huko Zanzibar ilimlazimu mke wake auze bangili ili apate uwezo wa kufanya kampeni.

Balozi Seif ameyasema hayo leo hii Jumamosi mjini Zanzibar  kwenye semina ya fursa ambapo amesema kuwa kama mgombea hana uwezo ni vigumu watu kumpigia kura kwani wapigakura wengi wanahitaji chochote

Pia Balozi Seif Ali Idd amesema alipata wakati mgumu sana alipoingia kwenye siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2005 kwa kuwa alikuwa mwanadiplomasia na kazi ya siasa inahitaji mtu ujipange sana.

Kuhusu kazi ya siasa, Balozi Seif amewata wale wote wanaofikiria kufanya kazi hiyo wajue ni kazi yenye changamoto nyingi.

“Fursa ya kisiasa sawa, njoo, lakini kuna changamoto, changamoto zenyewe zipo,kila baada ya miaka 5 lazima uwende ukawasujudie watu,” amesema Balozi Seif Ali Idd.

Vile vile, Balozi Seif Ali Idd ambae ni Mwakilishi wa jimbo la Kitope Zanzibar, amesema tofauti na hivyo ni vigumu kushinda kwani watu hawatakuelewa.

Balozi Seif Ali Idd amewataka vijana wasitegemee sana ajira za Serikali kwani huko nafasi ni chache hivyo amewahimiza wajibidishe katika kujiajiri kwani hata matajiri wengi walianza kwa shughuli ndogo ndogo na kujituma.

Nae Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jimbo la Mpendae Zanzibar, Salim Hassan Turky amewataka vijana wa Zanzibar wasione aibu katika kufanya biashara kwani hata matajiri wengi walianza kwa kufanya shughuli ndogo ndogo ambazo vijana wengi wanaona aibu kuzifanya.

Akijitolea mfano yeye mwenyewe, Turky amesema alianza kwa kuuza mifuko barabarani akiwa na umri wa miaka 8 hadi 9.

“Unamuona huyu Turky, kazi yangu kubwa ilikuwa ni kwenda katika nyumba zinazojengwa, naenda kuomba mifuko, sio nanunua, naomba mifuko ya saruji, siku zile mifuko ilikuwa ikiletwa nchini ilikuwa ni mifuko ya karatasi,” alisema Turky na kuongeza,

“Sasa unaenda unachukua mifuko ile, unakwenda unaikung’uta, ukisha ikung’uta unaitengeneza, ukishatengeneza, siku ya pili asubuhi kazi ni  mifuko ile unaweka kichwani,naanza kutembea Mkunazini mpaka Mlandege mpaka Mikunguni nauza mifuko ile  nikiwa na miaka 8,  9 nimeanza kazi hiyo,” amesema Turkyi.

Pia Turky amesema kuwa ili mtu aweze kufanikiwa ni lazima awe muaminifu na asiwe mjanja mjanja katika shughuli zake.

Turky maarufu “Mr White” anatajwa kuwa mongoni mwa wafanyabiashara wakubwa visiwani Zanzibar huku akimiliki Hoteli kadhaa na Hospitali iitwayo Tasakhtaa iliopo vsiwani humo.