Friday, August 14, 2020
Swahili > Habari > Habari za kimataifa > Antonio Guterres wa UN aisifu EAC

Antonio Guterres wa UN aisifu EAC

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, ameipongeza Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kufanya mambo yake kwa mpangilio mzuri, ikiwamo kusimamia mazungumzo ya amani nchini Burundi chini ya mpatanishi Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Alisema hayo alipokutana na Naibu katibu wa EAC anayeshughulikia shirikisho la kisasa ndani ya jumuiya, Charles Njoroge hivi karibuni katika makao makuu wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Akishukuru kwa niaba ya jumuiya, Njoroge alisema EAC inathamini amani, usalama na mazingira mazuri ya kuishi na pia inaheshimu haki za binadamu, kwani vyote kwa pamoja vinachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji kimaendeleo.

“Ndani ya jumuiya tunapenda kuona kila nchi inajikita kwenye shughuli za maendeleo pasipo na amani wala usalama huwezi kufanya maendeleo, ndiyo maana hatulali kuhakikisha nchi kama Burundi na Sudan Kusini zinaondoka kwenye machafuko.

Aidha alisema jumuiya inashukuru kwa jinsi inavyoungwa mkono na UN na AU katika masuala ya Burundi, huku akisema dhamira ya EAC ni kuona hata uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 unakuwa huru na wa haki.

Charles Njoroge, Naibu katibu wa EAC na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).

Alizungumzia maendeleo ya mikakati ya kurejesha wakimbizi kwao kutokana na makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi za EAC na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), alisema raia wengi waliokuwa wanaishi nje ya nchi yao kama wakimbizi wanarejea kwa kasi nyumbani Burundi.